NYUMBA YA HAKI YA ULIMWENGU
Oktoba 2019
Kwa wote ambao wamekuja kumuenzi Mtangulizi wa Mapambazuko mapya
Marafiki wapendwa Sana,
Tafakarini pamoja nasi. Pale Muelimishaji mtakatifu anapojitokeza ulimwenguni, Mtu maarufu Ambaye mafundisho Yake yatakuja kubumba fikra na vitendo vya binadamu kwa karne kadhaa zifuatazo—katika wakati huo wenye shauku na mitetemo, je, tungetarajia nini?
Kujitokeza kwa kila Muelimishaji kama huyo, kama ilivyoandikwa katika Vitabu Vitakatifu ya Imani kuu za ulimwengu, ni tukio la maana sana ambalo husukuma maendeleo ya ustaarabu. Kichocheo cha kiroho ambavyo kila mmoja amevitoa katika historia nzima kimewezesha kipenyo cha ushirikiano wa binadamu kupanuka kutoka ukoo, hadi kabila, hadi miji, na hadi taifa. Na kila mmoja wa Walimu hawa wakuu aliahidi kwamba, baada ya muda, Mtu mwingine mtakatifu angetokea, Ambaye ujio Wake ungetazamiwa na Ambaye ushawishi Wake ungeugeuza ulimwengu. Haistaabishi, basi, kwamba ujio wa Báb, Ambaye Kuzaliwa Kwake karne mbili zilizopita kunaenziwa sasa , kulileta msisimko usio wa kipekee katika nchi Alimozaliwa. Mara tu baada ya kujitokeza Kwake, kama ilivyokuwa kujitokeza kwa Watu maarufu kama hao, kuliharakisha uachiliwaji wa nguvu ya kiroho yenye uwezo --lakini hapakuwa na tamasha ambatani. Badala yake palikuwa na mazungumzo ya wakati wa jioni sana, katika makazi ya kawaida kabisa ya Muajemi, kati ya mwanafunzi wa dini na Mwenyeji wake kijana, wakati ambapo yule Mwenyeji aliweka wazi kwamba Alikuwa Ndiye Mwahidiwa, Muelimishaji mtakatifu ambaye mgeni Wake alikuwa akimtafuta. Tazama kwa makini,
Alitanabahi, Je, Mtu uliyemtarajia…anawezi kuwa mwingine zaidi ya Mimi?
Ni Kijana huyu, Báb, ambaye tungempokea kwa shangwe kama Mwahidiwa Ambaye kuja Kwake--baada ya kipindi cha miaka elfu moja--kwa mara nyingine tena kulitawanya mwanga wa uongozi mtakatifu juu ya ulimwengu wa binadamu.
Kutoka wakati huu yalikunjuka yale yote ambayo yamekuja kupita. Maandiko ya Báb yalitiririka kwa wingi kutoka katika kalamu Yake, yakifichua kweli za kina, yakiondosha ushirikina ambao ulisukasuka katika siku Yake, yakiwasihi watu kutambua umuhimu wa nyakati, yakiwaadhibu vikali kwa kukemea unafiki wa viongozi wao, na yakiuitia ulimwengu kwenye kiwango kilichotukuka cha mwenendo. Enyi watu wa ulimwengu!
Alitangaza katika mojawapo ya kazi Zake kuu, Hakika Mwanga ung’aao wa Mungu umetokea katikati yenu…ili muweze kuongozwa barabara kwenye njia za amani na, kwa idhini ya Mungu, mtoke gizani na kuingia katika mwanga na kwenye hii Njia Pana kabisa ya Ukweli.
Ushawishi Wake ulienea kwa haraka isiyo ya kawaida, ukifika mbali zaidi ya Uajemi. Watazamaji walishangazwa vile vile kwa idadi iliyoongezeka kwa haraka ya wafuasi Wake na kwa matendo yao ya ushujaa usioshindika na ibada. Matukio ya Maisha ya Báb--tao jepesi ililolifuatilia na mfululizo wa matukio ya huzuni ambayo yalihitimisha—yalisababisha roho jasiri kusafiri hadi Uajemi ili kuchunguza zaidi, na kuvutia mlolongo wa utukuzo wa kisanii kwa Utu Wake.
Mng’ao wa mwanga wa Báb huonekana mkali zaidi kiasi cha kutoona vizuri unapowekwa kwenye mazingira ya giza la kijamii ambamo Alitokea. Karne ya kumi na tisa Uajemi iliondolewa kabisa kutoka siku za utukufu wake wakati ustaarabu wake ulipokuwa husuda ya ulimwengu. Sasa ujinga umeigubika; mifumo ya imani isiyo na maana ilipitishwa bila kupewa changamoto; ukosefu wa usawa ulichochewa na ufisadi ulioenea pote. Dini, msingi wa zamani wa ustawi wa Uajemi, ikawa shirika lililonyang’anywa roho yake ihuishayo. Kila mwaka uliofuata uliupa umma uliotiishwa njozi na utovu wa matumaini tu. Ukandamizaji ulikuwa kamili. Kisha, kama vile tufani ya masika, Báb akaja kusafisha na kutakasa, kung’oa desturi potofu zilizotumika na kudhoofika za enzi na enzi, na kusafishia mbali vumbi lililozuia kutoka machoni pa wale waliopofushwa na njozi. Lakini Báb alikuwa na lengo maalum aliloliona. Alitafuta kuwaandaa watu kwa ajili ya kujitokeza kwa karibuni kwa Baha'u'lláh—wa pili kati ya Nyota Pacha zilizokusudiwa kuleta mwanga mpya kwa jamii ya binadamu. Hii ndiyo ilikuwa dhamira Yake aliyoisisitiza kabisa. Wakati Nyota ya Mchana ya Bahá itakapong’aa kwa wangavu juu ya upeo wa umilele
, Aliwaagiza wafuasi Wake, inawapasa kujiwasilisha nyinyi wenyewe mbele ya Kiti Chake cha Enzi.
Hivyo Báb na, kwa utukufu mkuu zaidi, Baha'u'lláh aliiangazia jamii na zama zilizogubikwa katika giza. Walizindua kipindi kipya katika mapinduzi ya kijamii: kipindi cha muunganiko wa familia nzima ya binadamu. Nguvu za kiroho Walizoziachilia ulimwenguni ziliingiza uhai mpya katika kila eneo la jitihada, ambapo matokeo yake yapo dhahiri katika mabadiliko ambayo yametokea. Ustaarabu wa kimwili umepiga hatua pasipo kukadirika; mafanikio mapya ya kustaajabisha katika sayansi na teknolojia yamefikiwa; malango kuelekea maarifa yaliyorundikwa ya binadamu yamefunguliwa wazi. Na kanuni zilizowekwa na Baha'u'lláh kwa ajili ya uinuaji na maendeleo ya jamii na kwa ajili ya kukomesha mifumo ya kikandamizaji na utengwaji zimepokelewa kwa mapana. Hebu fikiria mafundisho Yake kwamba jamii ya binadamu ni wamoja, au kwamba wanawake wapo sawa na wanaume, au kwamba elimu lazima iwe kwa wote, au kwamba utafutaji razini wa ukweli lazima uzishinde nadharia za kinjozi na chuki. Katika mataifa yote, sehemu kubwa ya watu wa ulimwengu hivi sasa wanakubaliana na tunu hizi za kimsingi.
Hata hivyo, mabishano dhidi ya tunu hizi, ambazo awali ziliwekewa mipaka kwa watu wenye fikra makini, pia yanazuka tena katika jamii--kumbusho kwamba mawazo bora huhitaji nguvu ya msimamo wa kiroho ili kuyaunganisha. Kwa kuwa ni jambo moja kukitambua kitu fulani kikanuni; na ni lingine kabisa kukikumbatia kwa moyo wote wa mtu, na bado ni vigumu zaidi kuipa tena jamii mtindo kwa namna ambayo hutoa maana ya pamoja. Bado hii ni shabaha ya jumuiya zinazoibukia kote ulimwenguni ambayo ambayo huelekeana na mafundisho ya Baha'u'lláh. Jumuiya hizi zinapambana kumakinikia mwanga wa mafundisho hayo kwenye matatizo sugu ambayo huitesa jamii zinazowazunguka; wanaandaa program za vitendo halisi zilizojikita juu ya maadili ya kiroho. Hizi ni jumuiya ambazo hulea elimu ya wote wawili wasichana na wavulana katika hali zozote zile; ambazo huchangia kwenye dhana ipanukayo ya ibada ambayo hujumuisha kazi ifanywayo kwa moyo wa huduma; ambazo hutazama kwenye lengo la kupata mambo bora ya kiroho, kuliko ubinafsi, kama machipuko yatiririkayo daima ya motisha; na ambazo hufundisha maafikiano ili kuendeleza mabadiliko ya mtu binafsi na ya kijamii. Zinatafuta kuleta maendeleo ya kiroho, kijamii na kimwili sambasamba. Zaidi ya yote, hizi ni jumuiya ambazo hujipambanua zenyewe kwa msimamo wao wa umoja wa jamii ya binadamu. Wanathamini utajiri wa anuwai zinazowakilishwa na koo zote za ulimwengu, wakati huo huo wakishikilia kwamba utambulisho wa mtu kama mshiriki wa mbari ya binadamu una mfano wa kurejelea kabla ya utambulisho na ushirika mwingine. Wanathibitisha haja ya utambuzi wa ulimwengu mzima, wakiinukia kutoka masuala ya pamoja kwa ajili ya ustawi wa jamii ya binadamu, na wanawahesabu watu wote wa dunia kama kaka na dada wa kiroho. Wakiacha kuridhika tu kuwa miongoni mwa jumuiya hizo, wafuasi wa Baha'u'lláh wanafanya jitihada endelevu kuzialika roho zenye mawazo sawa na wao kujiunga nao katika kujifunza jinsi ya kuyaweka mafundisho katika vitendo.
Hii hutuleta kwenye kiini cha jambo. Suala lililomo mikononi lina changamoto, na huhitaji uwazi. Kuna hoja nyingi nzuri na za ajabu ulimwenguni, na zinaibuka kutoka mitazamo maalum, kila moja ikiwa na sifa yake njema. Je, Hoja ya Baha'u'lláh ni mojawapo tu kati ya hizo? Au ni ya kiulimwengu, ikijumuisha mawazo bora kabisa ya binadamu wote? Hata hivyo, ni Hoja ambayo itakauwa chemchemi ya haki na amani ya milele—siyo kwa mahali pamoja au watu, bali ni kwa mahali pote na watu wote--lazima iwe isiyokwisha, lazima imiliki uhai wa kimbingu ambao huiwezesha kuvuka vizuizi vyote vinavyoizunguka kila kipimo cha Maisha ya binadamu. Hatimaye, lazima iwe na nguvu ya kugeuza moyo wa binadamu. Kisha, kama alivyokuwa mgeni wa Báb, hebu tuichunguze kwa makini. Je, Hoja ya Baha'u'lláh haina sifa hizi hizi?
Ikiwa mafundisho yaliyoletwa na Baha'u'lláh ndiyo yatakayoiwezesha jamii ya binadamu kusonga mbele hadi kwenye viwango vya juu kabisa vya umoja, basi mtu lazima aitafute roho kwa ajili ya muitikio sahihi. Makundi ya watu waliomtambua Báb waliitwa kwenye ushujaa, na muitikio wao mtukufu kabisa umeandikwa katika historia. Acha kila mmoja ambaye yupo macho kwa hali za ulimwengu, na kwa maovu yanayochagiza ambayo hutatanisha maisha ya wakazi wake, asikilize mwito wa Baha'u'lláh wa huduma isiyo na ubinafsi na thabiti--ushujaa kwa zama za sasa. Je, ni kitu gani kingine kitakachouokoa ulimwengu isipokuwa jitihada za roho zisizohesabika ambao huufanya ustawi wa jamii ya binadamu kuwa jambo lao kuu, wasi wasi yao itawalayo?
[Imesainiwa na: Nyumba ya Haki ya Ulimwengu]